Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain imeitaka Serikali ya Bahrain kusitisha mara moja hatua na vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya uhuishaji wa alama za kidini na misafara ya maombolezo, na kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kutekeleza ibada na kuhuisha alama zao za kidini kwa uhuru na kwa mujibu wa Katiba na mikataba ya kimataifa.
Jumuiya hiyo, katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, ililaani hatua na maamuzi ya kiholela ambayo yamesababisha kufutwa kwa shughuli katika maeneo 50 ya maombolezo (Husainiya) pamoja na misafara maalumu ya kuhuisha sherehe za maombolezo na matukio mengine. Ilisema kwamba hatua hizo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa ambazo Serikali ya Bahrain imesaini, hususan Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu, na Mkataba wa Kiarabu wa Haki za Binadamu.
Jumuiya ya Bahrain iliongeza kwamba; hatua hizi kwa hakika hazitenganishwi na mazingira ya jumla ambayo Bahrain imekuwa ikishuhudia hivi karibuni tangu kuanza kwa vita dhidi ya eneo hilo au hata kabla yake; bali ni hatua mpya katika mfululizo wa sera inayozidi kuwa kali, ambayo inalenga jamii ya Shia na katika kipindi cha hivi karibuni imehusisha mambo yafuatayo: kuzuia au kuweka vikwazo dhidi ya shughuli za ziara ya Arubaini, kuweka masharti magumu dhidi ya alama na maadhimisho yote ya kidini ya Shia, kuanzisha wimbi la kukamatwa kwa washiriki katika maandamano na mikusanyiko ya amani, sambamba na kukamatwa idadi kubwa ya wanazuoni wakubwa na maulamaa wa Shia, huku kukiwa na taarifa zilizothibitishwa kuhusu kufanyiwa vitendo vya ukatili, kutendewa vibaya na kuwekwa kizuizini kiholela; jambo linalothibitisha kuwepo kwa mfumo unaolenga kwa namna ya pekee haki za kidini na hata za kiraia za kundi hili la wananchi.
Jumuiya hiyo ilisisitiza: Mamlaka za Bahrain zinaendelea kufuata sera ya ukandamizaji wa kimfumo dhidi ya jamii ya Shia; sera ambayo kasi yake iliongezeka zaidi baada ya kuanza kwa uvamizi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sera hiyo inatekelezwa kupitia kuweka vikwazo vikubwa dhidi ya uhuishaji wa alama za kidini, ikiwemo kuzuia kuandaliwa kwa misafara ya maombolezo, kuzuia majlisi na maadhimisho ya kidini kufanyika nje ya maeneo ya maombolezo na Husainiya, na kusitisha shughuli zote za kidini katika muda maalumu.
Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain ilisema kwamba; hatua hizi zinatekelezwa kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa na Idara ya Wakfu wa Jaafari, ambayo imeshiriki kikamilifu katika sera za kiholela dhidi ya jamii ya Shia na haionyeshi chochote zaidi ya kuwa chombo cha utekelezaji kinachotumikia mamlaka.
Jumuiya hiyo ilisisitiza umuhimu wa kusitishwa kwa aina zote za ukandamizaji wa kiusalama dhidi ya maeneo ya maombolezo, Husainiya na taasisi za kidini. Pia ilitaka kusitishwa kwa kuwaita au kuwawekea shinikizo wasimamizi wa maeneo hayo kwa sababu ya kufanya shughuli zao za kidini, kusitishwa kwa ubaguzi wa wazi unaotokana na dini au imani, na kuhakikishwa kwa usawa wa makundi yote katika kufurahia haki na uhuru wa kutekeleza imani zao.
Jumuiya ya Bahrain imewataka waandishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Dini au Imani na waandishi Maalumu kuhusu Haki ya Uhuru wa Kukusanyika kwa Amani na Kuunda Vyama kufuatilia na kutathmini maendeleo haya, kufuatilia na kuweka kumbukumbu za ukiukaji unaoikabili jamii ya Shia nchini Bahrain, pamoja na kuwasiliana na mamlaka za Bahrain na kuzishinikiza kuheshimu wajibu wao wa kimataifa katika uwanja wa haki za binadamu.
Maoni yako